Mtazamo Mbadala

Friday, June 16, 2006

Karume kaingia Ikulu kwa ufunguo wenye kutu

Na Saed Kubenea

KILICHOFANYIKA Zanzibar katika uchaguzi wa rais, wawakilishi na madiwani uliofanyika Oktoba 30, ni sawa na mapinduzi ya kijeshi.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ilijiandaa kumbakiza Rais Amani Karume madarakani. Iliandaa mazingira ya kijeshi kwa ajili ya operesheni iliyopewa jina ‘uchaguzi.’

Idadi kubwa ya majeshi yaliyomwaga Zanzibar iliashiria jambo moja tu, kwamba Rais Karume alijiandaa kufanya mapinduzi. Alijua angeshindwa, kaamua kuandaa mazingira ya vitisho dhidi ya wananchi.

Ulikuwa ujumbe kwamba wamchague, wamchague, ni yeye tu angeingia Ikulu. Ndiyo maana hatukatai kwamba mbele ya mitutu mingi iliyotapakaa mitaani kiasi hicho, dhana kwamba wapo wengi walioshindwa kupiga kura.

Na si kwamba walishindwa, bali waliogopa kwenda vituoni. Waliogopa risasi. Wapo pia walioghairi, kwamba mambo yenyewe kama ndiyo haya, ni bora kutopiga kura kabisa.

Kauli za Karume zinaweza kuthibitisha hoja kwamba alidhamiria kumpindua mshindani wake kama tume ingemtangaza mshindi. Kwani alikuwa na maana gani aliposema anajua ulipo ufunguo wa baba yake? Ufunguo gani huo kama si wa mapinduzi?

Ni kweli, baada ya uchaguzi, Wazanzibari wameuona ufunguo wa baba yake. lakini ufunguo wenyewe umeshaota kutu. Unaweza kufungua mlango. Na tayari Karume anautumia kufungulia mlango wa Ikulu. Lakini kinachodhihirika sasa ni kwamba ufunguo huo umepata kutu. Utakatika.

Inashangaza kwamba taifa linatumia mabilioni ya pesa kuandaa na kufanya uchaguzi feki, huku taifa hilo hilo likijua kwamba si kura bali ufunguo wenye kutu ndio utatumika kufungulia milango ya Ikulu.

Watu wastaarabu wanasema huu ni uhuni. Na kama siasa zetu zinageuzwa za kihuni, kuna haja ya kuziita siasa?

Kinachokera zaidi ni pale hata wanaojiita na kuitwa waangalizi wa nje wanaposifia uozo, wakadai umefanyika uchaguzi huru na wa haki Zanzibar. Uhuru katikati ya mitutu na vitisho vya aina ile? Uhuru gani? Haki inapatikana wapi iwapo watu wanapiga kura mara mbili, tatu nne, katika vituo tofauti?

Kuna uhuru gani katikati ya vitisho vya Janjaweed na askari wa JKU, KMKM na polisi? Kuna haki gani katika kuwaruhusu wakazi wa Tanzania Bara kujiandikisha na kupiga kura katika uchaguzi wa Zanzibar?

Maana wapo, na sasa wanajisema wenyewe. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliandaa makada kadhaa jijini Dar es Salaam, nao wakaandaa vijana hamsini hamsini, wakalipwa pesa nzuri, wakatangenezewa vitambulisho na kupelekwa Unguja; wakapiga kura!

Kura za watu wa Tanzania Bara nazo zimehesabiwa katika zile zinazodaiwa kumweka Rais Karume madarakani. Eneo lake la utawala linaishia wapi?

Ona maajabu ya funguo wa Karume. Kapata ushindi wenye utata na kutangazwa rasmi alasiri ya Jumanne. Jumatano asubuhi, saa tatu, tayari ameapa.

Maandalizi ya sherehe yamefanywa saa ngapi? Mialiko ya waliohudhuria sherehe za kualikwa Karume ilisambazwa lini? Imejibiwa lini?

Kwa mantiki hii, kwa nini watu wasidhani kwamba mkakati wa ‘ushindi’ wa Karume haukuwahusisha wanachama na viongozi wa CCM pekee?

Wawe wa nje au wa ndani ya nchi, wowote walioshiriki sherehe za kuapishwa kwa Karume, na wote waliotoa taarifa kwamba uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa huru na wa haki, ni washiriki katika mchakato uliomweka Karume madarakani. Kama CCM isivyoaminika tena mbele ya wananchi, nao hawaaminiki.

Tunaelewa waangalizi wa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wanapotoa taarifa yao na kusema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki. Hawa ni makonredi wa Rais Mkapa na Karume. Kama ilivyo kawaida kwa viongozi wetu wa Afrika, hakuna kukemeana na kukosoana hata yafanyike madudu gani.

Hakuna kiongozi hata mmoja katika SADC mwenye uwezo wa kumnyoshea kidole Rais Mkapa. Hayupo! Kwa hiyo, taarifa zao hazishangazi.

Lakini kusema ukweli hakuambatani na mamlaka ya msemaji. Ile ni dhamana itokayo kwa Mungu, ambayo hutambulika kwa kutumia milango ya fahamu aliyotujalia, ikiongozwa na utambuzi wa kiakili.

Hawa na wote wametenda dhambi isiyosameheka. Dunia inawashangaa, CCM inawapongeza!

Imesikitisha kwamba miongoni mwa walioimba wimbo ule ule yumo Msajili wa Vyama vya Siasa. John Tendwa. Naye anasema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.

Amekwisha. Hana tena uadilifu wa kuvisimamia vyama vingine vya siasa. Ameshakuwa mbaguzi. Hataheshimika, hata kwa wale anaowapendelea. Sana sana watamwona kibaraka na mtu anayejipendekeza.

Maana haiwezekani msomi wa viwango vya Tendwa kufikia mahali pa kutotambua tofauti kati haki na dhukuma; uhuru na utumwa.

Kwa kuwa naye kawa mshiriki katika dhuluma, na Watanzania wamesikia, ameshiriki katika kubomoa hata kile kidogo kilichokuwapo.

Ndiyo. Watawala wanaing’ang’ania Zanzibar, lakini kisiwa hiki bila kuwa na siasa za kiungwana na za haki, kitaisambaratisha Tanzania. tunakoelekea si kwenye neema.

Mwisho.

Sunday, June 11, 2006

Wasomi vihiyo

Nimefurahishwa sana na mjadala unaopatikana katika blgger ya Mnyika, kuhusiana na Vihiyo na hatma ya Tanzania. Ni kweli kwamba, Tanzania kama taifa inakabiliwa na kubarua kigumu cha kusonga mbele katika kalne hii ya Sayansi na Tekronojia kutoka na kuendeshwa na wanasiasa na watawala vihiyo.

Kwa hakika, vihiyo wapo wengi sana hapa nchini na wameenea kila fani ikiwam0o fani ya habari. Baadhi yao, ni Wahariri na wengine ni Wakurugenzi. Kutokana na ukihiyo wao, wameshindwa kufanya kazi ya umma. Wameshindwa kusimama wenyewe. Sasa wanasaka huruma kutoka kwa baadhi ya watawala.

Hali imekuwa mbaya zaidi baada ya baadhi ya wasomi wetu vihiyo, sasa kuendesha biashara ya baa. Ni wazi kuwa wameamua kufanya biashara hiyo baada ya kushindwa kufanya kazi za kiutafititi. Ukitaka usahidi wa hilo, nenda mkoani Mororgoro, Mashariki mwa Tanzania. Kila kona utakutana na baa za wasomi vihiyo. Kila baa nzuri iliyopo katika kona ya mkoa huo, utaambiwa hii ni ya Profesa fulani yupo SUA. Hii ni ya Profesa fulani yupo Mzumbe. Hii ni ya Dk. fulani yupo SUA na hii ni ya Dk. fulani yupo Mzumbe na kadhalika na kadhalika.

Kuna habari kuwa yupo Wazirimmoja wa JK, ambaye ana shahada ya Udaktari ambao Mnyika anautilia mashaka pia anayo baa yake katikati ya mkoa huo.Nasikia sasa, baadhi ya vihiyo hawa kutokana na kupendwa kujikweza wanataka hata wahudumu wao wawe na sifa ya elimu ya chuo kikuu.

Kutokana na tabia ya wasomi hawa vihiyo ya kujikweza, muda si mrefu Watanzania watashuhudia nafasi za uhudumu katika baa zao zishikwe na wasomi wenye shahada ya chuo kikuu. Mungu aepushie mbali!

Najua kwamba, kufanya biashara ya baa kwa mtu yoyote si kosa. Lakini ni wazi kwamba kwa msomi ambaye anatakiwa kutumia muda wake mwingi kufanya utafiti, kufundisha na kuelimisha, kufanya biashara hii, ambayo inamlazumu kutumia muda wake mwingi kufuatalia vinywaji na wateja, ni kujidhalilisha.

Mungu inusuru Tanzania.